Monday, January 7, 2013


Mcheza kiungo wa Manchester City Yaya Toure ametangazwa kuwa mshindi wa tuzo ya mchezaji bora barani Afrika kwa mwaka wa pili mfululizo.
Toure alimshinda noadha wa Ivory Coast na mshambulizi wa zamani wa Chelsea Didier Drogba na aliyekuwa mlinda lango wa Arsenal Alex Song.
Drogba alimaliza katika nafasi ya pili naye Song akawa wa tatu, katika uteuzi uliofanywa na makocha na maafisa wa kiufundi wa timu za soka barani Afrika ambazo ni wanachama wa shirikisho la mchezo wa soka barani Afrika CAF.
Aliyekuwa mshambulizi wa Barcelona Samuel Eto'o ndiye anayeshikilia rekodi ya kushinda tuzo hiyo mara nyingi.  Eto'o ameshinda tuzo hiyo mara nne.
Mabingwa wa soka barani Afrika, Zambia walituzwa kuwa timu bora barani mwaka huu na kocha wao Herve Renard naye aliteuliwa kuwa kocha wa mwaka.
Song kwa sasa anaicheza klabu ya Barcelona naye Drogba anaicheza klabu ya Shanghai Shenhua ya Uchina tangu mwezi Mei Mwaka huu.
Toure, ambaye alishinda tuzo hiyo mwaka uliopita, ni miongoni ma wachezaji wa timu ya taifa ya Ivory Coast, wanaoelekea nchini Afrika Kusini mwa michuano ya kombe la Mataifa Bingwa Barano Afrika itakayoanza mwezi ujao.

ZUMA ATUMA WANAJESHI BANGUI


Afrika Kusini imethibitisha kwamba imetuma wanajeshi zaidi huko Jamhuri ya Afrika ya Kati huku wapiganaji wanaendelea kusonga dhidi ya serikali. Msemaji wa wizara ya mashauri ya nchi za nje mjini Pretoria alieleza kuwa wanajeshi 120 zaidi wametumwa kulinda wanajeshi wa Afrika Kusini ambao tayari wako Jamhuri ya Afrika ya Kati kulifunza jeshi la serikali. Ofisi ya Rais Zuma inasema kuwa serikali imeidhinisha jumla ya wanajeshi 400 kutumwa huko. Wapiganaji na serikali ya Jamhuri ya Afrika ya Kati wanatarajiwa kuanza mazungumzo katika siku za karibuni.

MAGAZETI YA LEO 07/01/2013








SYRIA


Rais Bashar al-Assad wa Syria Jumapili (06.01.2013) amefuta uwezekano wa mazungumzo na makundi ya upinzani ambayo ameyaita kuwa “vibaraka” wa mataifa ya magharibi na ameapa kupambana na “magaidi” na “magenge ya wahuni.”
Al-Assad amesema katika hotuba yake ya kwanza kwa umma baada ya zaidi ya miezi saba kwamba hao ni maadui wa wananchi, maadui wa Mungu na wameamuwa kufanya ugaidi kwa kuwatisha wananchi.
Ameongeza kwamba wanayaita hayo mapinduzi lakini wanachokifanya hakihusiani kabisa na mapinduzi kwani mapinduzi yanahitaji watu wenye fikra wakati watu hao ni kundi tu la wahalifu.Wafuasi wake waliokuwa kwenye ukumbi wa jengo la michezo ya kuigiza mjini Damascus walimkatiza mara kwa mara kwa kumshangilia kwa mayowe “Kwa roho na damu yetu tutakulinda Assad”.
Al-Assad amesema waasi wanaoungwa mkono na mataifa ya kigeni wanaendesha vita nje ya nchi hiyo dhidi ya Syria.Akisisitiza madai ya serikali yake kwamba magaidi wa kigeni wanahusika na mzozo wa miaka miwili wa nchi hiyo amesema kwamba kilicho yakini ni kwamba wale wanaopambana nao hivi leo ni wale wenye kufuata itikadi ya Al Qaeda.Al-Assad ametowa wito kwa kujiandaa kwa taifa kuihami nchi hiyo kwa kile alichokiita kuwa “hali ya vita kwa maana halisi ya neno lenyewe.”
Amezishukuru Urusi,China na Iran ambazo ni washirika wake wakuu.

MAKUBALIANO YA NCHI ZA SUDAN


Kutoka DW Swahili, taarifa ikufikie kwamba Marais wa Sudan na Sudan kusini wamekubaliana kuhusu muda utakaopangwa kwa ajili ya utekelezaji wa masuala muhimu wakati walipokutana kwa faragha katika mji mkuu wa Ethiopia, Addis Ababa.
Usalama, mafuta na mipaka ni miongoni mwa masuala ambayo rais wa Sudan ya kusini Salva Kiir na mwenzake wa Sudan Omar Hassan al – Bashir waliyajadili Addis Ababa kwa upatanishi wa umoja wa Afrika.
Pande hizo mbili zimekubaliana kuwa makubaliano yaliyofikiwa katika mkutano uliofanyika septemba 2012 yanapaswa kutekelezwa bila masharti yoyote, amesema mpatanishi wa umoja wa Afrika ambae ni rais wa zamani wa Afrika kusini Thabo Mbeki ambae amekaririwa akisema “Jopo letu linatayarisha utaratibu wa utekelezaji wa makubaliano yote yaliyokwisha fikiwa kwa kupanga muda maalum”