Monday, January 7, 2013

SYRIA


Rais Bashar al-Assad wa Syria Jumapili (06.01.2013) amefuta uwezekano wa mazungumzo na makundi ya upinzani ambayo ameyaita kuwa “vibaraka” wa mataifa ya magharibi na ameapa kupambana na “magaidi” na “magenge ya wahuni.”
Al-Assad amesema katika hotuba yake ya kwanza kwa umma baada ya zaidi ya miezi saba kwamba hao ni maadui wa wananchi, maadui wa Mungu na wameamuwa kufanya ugaidi kwa kuwatisha wananchi.
Ameongeza kwamba wanayaita hayo mapinduzi lakini wanachokifanya hakihusiani kabisa na mapinduzi kwani mapinduzi yanahitaji watu wenye fikra wakati watu hao ni kundi tu la wahalifu.Wafuasi wake waliokuwa kwenye ukumbi wa jengo la michezo ya kuigiza mjini Damascus walimkatiza mara kwa mara kwa kumshangilia kwa mayowe “Kwa roho na damu yetu tutakulinda Assad”.
Al-Assad amesema waasi wanaoungwa mkono na mataifa ya kigeni wanaendesha vita nje ya nchi hiyo dhidi ya Syria.Akisisitiza madai ya serikali yake kwamba magaidi wa kigeni wanahusika na mzozo wa miaka miwili wa nchi hiyo amesema kwamba kilicho yakini ni kwamba wale wanaopambana nao hivi leo ni wale wenye kufuata itikadi ya Al Qaeda.Al-Assad ametowa wito kwa kujiandaa kwa taifa kuihami nchi hiyo kwa kile alichokiita kuwa “hali ya vita kwa maana halisi ya neno lenyewe.”
Amezishukuru Urusi,China na Iran ambazo ni washirika wake wakuu.

No comments:

Post a Comment